Media Centre
Speech
Dar es Salaam Oye, Dar es Salaam Oye!
Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri wetu na Wizara yake, pamoja na Wageni wetu wote waalikwa, Mabibi na Mabwana. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Kazi Iendelee!
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nashukuru kwa kuchagua Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa tukio hili. Nimeona kaulimbiu kuu ya mwaka huu, ambayo imenipeleka mbali, na kwa kifupi, nasema hivi: Masuala ya Artificial Intelligence, kwa lugha nyepesi ni kama kuiwezesha kompyuta au mashine kufikiri, kuelewa, na kutenda kama binadamu. Kwa kufanya hivyo, taaluma ya falsafa ina matawi yake, na tawi la kwanza linaitwa axiology, ambalo linafuatilia chimbuko na mabadiliko ya jambo. Matawi mengine ni mantiki (logic), epistemology, metaphysics, falsafa ya kisiasa, maadili (ethics) na mengine mengi.
Moja ya mambo muhimu kuhusu artificial intelligence ni uwezo wa kuzipa mashine uwezo wa kufikiri, na katika taaluma ya falsafa, kufikiri kunaangukia kwenye mantiki. Ikiwa mashine zitapata uwezo wa kufanya kazi kama binadamu, basi uwezo wa binadamu utakaribia kuwa sawa na kile anachokivumbua.
Hii ina maana kwamba msingi mkubwa wa artificial intelligence unaanzia kwa binadamu mwenye uwezo wa kufikiri kwa ufasaha, kugundua na kuvumbua, ili mwisho wa siku tuweze kupata sayansi inayolingana na anavyoweza kufikiria.
Nashukuru kwa kile tulichojifunza hapa, mambo makubwa na muhimu. Jambo moja kubwa ambalo nimeona ni kwamba kongamano hili limeendeshwa kwa Kiswahili. Tukiendelea kutumia Kiswahili, watu wengi wataendelea kuelewa na kuwa na uwezo wa kuwasilisha kile tulichojifunza. Hii ni kwa sababu tunaumiliki na ustadi wa Kiswahili hapa Tanzania, na hilo linatusaidia kupata maarifa, ujuzi, na kuwasiliana kwa urahisi kuhusu mada muhimu kama hii.
Nawakaribisha tena mkoani Dar es Salaam, na ninawahakikishia mkoa wetu ni salama kwa yeyote kuishi hapa. Wageni ambao mmetoka mbali, Dar es Salaam ni jiji kubwa sana, lenye idadi ya watu takriban milioni 5.3 kwa mujibu wa sensa ya mwaka jana. Mkiwa na muda, nawaalika kutembea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa. Nina hakika kwamba mtavutiwa na tutafanya kila jitihada kuhakikisha mnaondoka na furaha mliyokuja nayo.
Asanteni sana!
Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi mbalimbali mliokuwepo hapa, hitifaki ikizingatiwa.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nina jukumu moja tu ambalo ni kufanya utambulisho wa wageni waliokuwepo ndani ya ukumbi huu.
Naomba nianze na kutambulisha meza kuu:
Kwanza, tunaye Mheshimiwa Jerry William Slaa (Mbunge), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; Mheshimiwa Nados Bekele Thomas, Mtendaji Mkuu wa AUDAT-NEPAD; Mheshimiwa Suleiman Kakoso, Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu; na Dr. Nkundwe Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kundi la pili ni Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri, wakiwemo Mheshimiwa Mary Priscus Maundi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na Dr. Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Afya.
Kundi la tatu ni Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, wakiongozwa na Mheshimiwa Mohammed Mohammed Ali. Pia tunaye Mheshimiwa Godfrey Mwambe, na Bi. Genesis Malangu, Katibu wa Kamati hiyo.
Kundi la nne ni Makatibu Wakuu na Manaibu wao, wakianzia na Bw. Bryson Msigwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo; Bw. Nicholas Mkapa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Balozi Saidi Musha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Dr. Hussein Mohammed Omad, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo; na Dr. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi.
Kundi la tano linahusisha Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakiongozwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Viongozi wa Wilaya, na Viongozi wa Dini.
Kundi la sita ni Waheshimiwa Mabalozi, Wanadiplomasia, na Wakuu wa Misimu mbalimbali wanaowakilisha nchi zao, taasisi, na mashirika ya kitaifa. Naomba niwataje wakuu wa maendeleo ya biashara wa Arabic Bank for Economic Development in Africa-BADEA, Bw. Cedric Montecho; Balozi wa Italia; Balozi wa Finland; Balozi wa Libya; Balozi wa Pakistani; Balozi wa Korea; Balozi wa Heshima wa Lithonia; Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia; Balozi wa Sudan; Balozi wa Urusi; Balozi wa Msumbiji; Balozi wa Qatar; na wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa pamoja na UNESCO.
Kundi la saba ni Uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ukiongozwa na Bw. Thobias Makoba, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari.
Kundi la nane ni Wenyeviti wa Bodi za taasisi zilizo chini ya wizara, wakiongozwa na Prof. Leonard James Msele, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Meja Generali Mstaafu Gaudence Salim Milazi, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF); Mheshimiwa Balozi Adad Rajab, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi; na Bi Khawa Ngombi, Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA-CCC.
Kundi la tisa ni Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Tunaye Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dr. Jabir; Mkuu wa Shirika la Mawasiliano (TTCL); Mkuu wa Shirika la Posta (TPC); Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF); Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi; Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania; Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania; na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano.
Kundi la kumi ni Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi wote waliopo.
Kundi la kumi na moja linajumuisha wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka wizara, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, wakala za serikali, idara zinazojitegemea, na taasisi za umma kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Uwepo wa Vyuo vya Elimu ya Juu vinavyofundisha taaluma ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, watoa mada mbalimbali, watoa huduma za lugha za alama, watoa huduma za afya, na wakalimani wa lugha za Kiingereza na Kiswahili.
Pia tunawashukuru wafadhili wa kongamano hili ambao ni Huawei, UNDP, na wadhamini wengine wote.
Kundi lingine ni waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari.
Na kundi la mwisho ni burudani, yani Brass Band.
Baada ya hapo naomba kuwakilisha kwa Waziri Mkuu, itifaki ikizingatiwa!
Mheshimiwa Mhandisi Mary Prisca Mahundi, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bwana Muhammed Hamis Abdula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na timu ya Menejimenti iliyoko hapa. Profesa Leonard Msele, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume yetu ya TEHAMA, pamoja na wajumbe wa Bodi mlioko hapa. Dr. Nkundwe Mosses Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA na menejimenti yako mlioko hapa. Waheshimiwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, natambua uwepo wa Balozi anayewakilisha Jumuiya ya Ulaya, Mheshimiwa Balozi wa Finland, Italia, Mwakilishi Mkazi wa UNESCO, Bwana Michael Toto, Dr. Greek Dawn ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania, na ndiye Mdhamini wetu mkuu kwa siku ya leo. Wakuu wa Taasisi za Serikali na sekta binafsi mlioko hapa, Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi za Umma mlioko hapa, wadhamini wetu, washiriki wa kongamano kutoka sekta za umma na binafsi, na wale wanaotufuatilia kupitia matangazo ya moja kwa moja. Wageni waalikwa, waandishi wa habari, mabibi na mabwana, nawasalimu kwa jina la Muungano wa Tanzania… kazi iendelee!
Ndugu washiriki, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha siku ya leo tukiwa na afya njema, na kutuwezesha kushiriki katika Kongamano la Nane la TEHAMA. Pili, namshukuru na kumpongeza Bwana Muhammed Hamis Abdula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na kamati nzima ya maandalizi ya kongamano hili - hongereni sana!
Pia kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya wana TEHAMA kutoka sekta ya umma na binafsi, niseme nimefarijika sana kuwa sehemu ya Jumuiya hii, ambayo pia mimi ni sehemu yake. Nilikuwa naangalia huku kwenye hadhara na nikajiuliza jinsi nitakavyoweza kuwa sehemu ya jumuiya hii. Nimemuona mwanafunzi mwenzangu Tatu Mikdadi, na nadhani kuna wengine pia wako katika sekta mbalimbali, nawashukuru sana!
Ndugu washiriki, ninawashukuru wadhamini na wadau wote wa maendeleo ya miundombinu ya TEHAMA, ubunifu katika TEHAMA, kuendeleza ujuzi na ubunifu katika TEHAMA, watafiti katika TEHAMA, wawekezaji na wadau wote kwa uwepo wenu hapa na kufanikisha shughuli hii muhimu kwa leo.
Nichukue nafasi hii kuwapongeza mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali na washiriki wa kimataifa ambao mmeona umuhimu wa kutenga muda wenu ili kuhakikisha kongamano hili la nane linafanikiwa. Karibuni sana! Nategemea kuwaona katika makongamano mengine yajayo!
Ndugu washiriki, wizara ninayoiongoza, pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kusimamia Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016, ambayo imeainisha masuala ya kisera, kisheria, na taasisi katika kukuza sekta ya TEHAMA nchini. Katika kutekeleza sera ya TEHAMA, Serikali kupitia amri ya Rais, iliunda Tume ya TEHAMA ambayo ilipewa majukumu yafuatayo:
- Kusimamia utekelezaji wa Sera ya TEHAMA.
- Kukuza uwekezaji katika sekta ya TEHAMA.
- Kujenga uwezo na kukuza utaalamu katika fani ya TEHAMA.
- Kushirikiana na wadau wengine katika masuala ya utafiti.
Ndugu washiriki, utekelezaji wa majukumu haya ndio umesababisha kuwepo kwa kongamano hili, ambapo wadau na wataalamu mbalimbali wanapata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha utekelezaji wa Sera ya TEHAMA nchini, lakini pia kuweka mikakati ya kwenda sawa na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoibuka, hasa katika nyanja za akili bandia, roboti na uchambuzi wa takwimu kubwa (Big Data Analytics).
Ndugu washiriki, nimejulishwa kuwa kongamano hili ni la nane tangu kuanzishwa kwa Tume ya TEHAMA. Pia nimejulishwa kuwa kongamano hili limetanguliwa na mkutano wa wanawake wanaoshiriki katika TEHAMA pamoja na vijana wanaojihusisha na TEHAMA, ambapo masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya TEHAMA yalijadiliwa.
Leo hii nitafungua kongamano hili ambalo lina kaulimbiu isemayo "Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Roboti kwa Mapinduzi ya Kijamii na Kiuchumi." Kaulimbiu hii inafungua mjadala muhimu sana, kwa wakati huu ambapo dunia nzima inashuhudia mapinduzi ya kidijitali.
Sisi kama taifa tunayo nafasi ya kutumia teknolojia hizi ili kuboresha ustawi wa wananchi wetu na kuongeza tija katika uchumi. Ndugu washiriki, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kupiga hatua kubwa katika TEHAMA, ambayo ni nguzo kuu ya kufikia uchumi wa kidijitali - yaani, Digital Economy.
Dunia hivi sasa ipo katika mapinduzi ya nne, tano na sita ya viwanda, yaani Mapinduzi ya 4th, 5th, na 6th Industrial Revolution, ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji kwa kiasi kikubwa zinakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za TEHAMA.
Kwa umuhimu huo, serikali imeendelea kuwekeza katika kufanya maboresho ya kisera, kisheria na kitaasisi pamoja na kujenga uwezo kwa Watanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa sehemu ya mabadiliko katika masuala ya TEHAMA duniani.
Ndugu washiriki, tumeshuhudia namna ambavyo akili mnemba na roboti zina uwezo wa kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wetu kwa njia ambazo zilikuwa hazifikiriki miaka michache iliyopita. Nimetembelea mabanda mbalimbali na kujionea namna ambavyo teknolojia ya akili mnemba na roboti inaweza kutumika katika sekta mbalimbali kama vile afya, ambapo akili mnemba na roboti vinaweza kusaidia kutoa utambuzi wa haraka wa magonjwa na kuboresha huduma za afya msingi.
Katika sekta ya kilimo, akili mnemba na roboti zinaweza kuboresha tija kwa wakulima kwa kusaidia katika usimamizi bora wa uzalishaji na utafiti wa hali ya hewa. Pia teknolojia hii inaweza kubadilisha kabisa jinsi tunavyoendesha biashara na utengenezaji wa bidhaa kwa kuboresha mifumo ya usambazaji na kuongeza ufanisi.
Kwa kutumia akili mnemba na roboti, viwanda vyetu vinaweza kuongeza uzalishaji na kuwa na ushindani katika soko la kimataifa. Aidha, akili mnemba na roboti zinaweza kuimarisha mifumo ya elimu kwa kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa kila mwanafunzi bila kujali eneo au hali yake ya kiuchumi. Kwa njia hii, tunaweza kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya kujifunza na kuchangia katika maendeleo ya taifa letu.
Ni matumaini yangu kuwa kongamano hili litawezesha kujifunza zaidi na kupata uzoefu katika matumizi sahihi ya akili mnemba na roboti ili kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma katika maeneo yetu.
Ndugu washiriki, nimejulishwa kuwa katika kongamano hili kulikuwa na maonyesho ya roboti kutoka kwa wanafunzi wa sekondari ambao wameonyesha ubunifu mkubwa na uwezo wa hali ya juu katika teknolojia. Nimejulishwa pia kuwa wanafunzi hao hawakutoka tu kwenye shule za mchepuo wa Kiingereza, lakini pia mchepuo wa Kiswahili kama vile shule za Azania, Jangwani, na Tambaza.
Kitendo hiki cha wanafunzi kutoka shule mbalimbali kuonyesha ubunifu wao kimeonyesha ukuaji wa teknolojia na uwezo wa kidijitali nchini. Inaonyesha kuwa shule zote na wanafunzi wa shule zote wana uwezo wa kuonyesha vipaji vyao katika ubunifu. Ninawaelekeza ICTC kuwasaidia kuwalea, lakini pia kuwasimamia wanapojiandaa kuelekea mashindano yatakayofanyika nchini Uturuki ili uwezo wao uweze kuonekana na kuleta matokeo bora na ushindi kwa Taifa letu.
Tanzania, kama ilivyo kwa nchi zingine zinazoendelea, inakabiliwa na changamoto hasa kwenye jamii zetu ambazo zinahitaji suluhisho la haraka na endelevu. Teknolojia za akili mnemba na roboti zinaweza kutusaidia kutatua changamoto hizi kwa kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kuleta ubunifu katika sekta mbalimbali kama nilivyosema hapo awali: sekta ya afya, kilimo, elimu, na usimamizi wa rasilimali.
Kwa hiyo, kongamano hili ni fursa ya kutafakari na kujadili hatua za kuchukua ili kuhakikisha kuwa teknolojia hizi zinatumiwa vyema kwa manufaa ya Taifa bila kuathiri masuala ya kiuchumi, kiusalama na tamaduni zetu.
Ndugu washiriki, ni matarajio yangu kuwa baada ya kongamano hili tutapata taarifa inayojumuisha maono yenu kuhusu maendeleo ya TEHAMA, pamoja na mapendekezo ya namna ya kuboresha sera na sheria zetu za kisekta ili kuweza kuchochea ukuaji na matumizi ya TEHAMA katika kuchangia pato la Taifa na kutoa huduma kwa wananchi.
Ndugu washiriki, baada ya kusema hayo, natangaza rasmi sasa kwamba Kongamano la Nane la TEHAMA kwa mwaka 2024 limefunguliwa rasmi!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
Mheshimiwa Waziri wetu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry William Slaa ambaye ni Mbunge, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Marry Prisca Maundi.
Naomba kutambua uwepo wa kila mmoja wetu hapa kama tulivyotambulishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA. Naomba niwasalimu kwa jina la Muungano wa Tanzania… Kazi Iendelee!
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kabla ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu wa Rehema, kwa kutuwezesha sote kukutana hapa leo asubuhi katika kongamano la TEHAMA la nane la mwaka 2024.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kongamano hili ni la kipekee kwa sababu lina uwakilishi mkubwa wa mabalozi kutoka nchi mbalimbali. Hatukuwahi kuwa na kongamano lenye uwakilishi mzuri wa kimataifa kama huu wa mabalozi. Kwa mantiki hiyo, kongamano hili limepata sura ya kimataifa, ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki. Tutaweza kushuhudia katika kongamano hili utoaji wa Tuzo ya Kimataifa, ambapo Tanzania imepata heshima ya kuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa mashindano yaliyoandaliwa na Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya akili mnemba na roboti.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tuzo hizo zitatolewa kesho kutwa ambapo mgeni rasmi atakuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, lengo kuu la kongamano hili ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya TEHAMA na kujadili masuala yanayohusu TEHAMA kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya TEHAMA nchini. Kwa kutambua umuhimu wa kongamano hili, kama tulivyoelezwa na Mkurugenzi Mkuu, litafanyika kwa siku tano. Tulianza na siku ya Wanawake na TEHAMA, tukaendelea na siku ya Vijana na TEHAMA jana, na leo hii unatufungulia rasmi kongamano hili. Hivyo, kongamano litaendelea hadi siku ya kufunga rasmi, kesho kutwa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kujumuishwa kwa makundi haya mbalimbali katika jamii, ikiwemo siku maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana, kumetoa nafasi ya kujadili masuala yanayohusu teknolojia zinazoibukia.
Kaulimbiu ya kongamano hili ni Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Roboti kwa Ajili ya Mapinduzi ya Kijamii na Kiuchumi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, mada mbalimbali kama alivyoelezea Mkurugenzi Mkuu zimejadiliwa kuhusu matumizi ya akili bandia katika kutoa huduma mbalimbali kwenye sekta za afya, elimu, kilimo na kadhalika. Ndiyo uzuri wa kongamano hili, Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ambapo tuna mada nyingi kutoka kwa watoa mada kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya, na kwa hivyo, tuna sura nzima ya ulimwengu hapa.
Ni fursa kubwa tuliyoipata katika wiki hii ya siku tano kwa lengo la kujifunza na kuendelea kujifunza. Kama tunavyojua sote, dunia inaelekea kwenye teknolojia, hasa teknolojia zinazoibukia.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, wajibu wangu mkuu niliposimama hapa ni kukukaribisha wewe hasa. Nimeona ni vema nitoe maneno haya machache ya utangulizi kabla sijakukaribisha.
Basi, baada ya kusema hayo, sasa naomba kwa unyenyekevu kabisa nichukue fursa hii kukukaribisha wewe kuja kutoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano hili la nane la TEHAMA.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, karibu sana!