THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

INFORMATION AND COMMUNICATION TECHNOLOGIES COMMISSION

Wataalamu TEHAMA Wavutiwa Na Mafunzo Estonia

  • News

WATAALAMU wa TEHAMA waliopo kwenye ziara ya siku tano ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na usalama nchini Estonia wamezungumzia umuhimu wa mafunzo hayo sambamba na mwelekeo wa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kujenga uchumi wa kidigitali.

Akizungumzia ziara hiyo ya kujifunza inayoendelea katika Jiji la Tallinn nchini humo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt Nkundwe Moses Mwasaga ambaye ameongoza timu wataalamu kumi kutoka taasisi mbalimbali za umma amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo mkubwa.

“Wenzetu Estonia wamebobea sana katika masuala ya TEHAMA na ziara yetu hapa itasaidia sana kuwajengea uwezo wataalamu wetu. Ni mwelekea serikali ya awamu ya sita kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya TEHAMA na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidigitali,” alisema Dkt Mwasaga.

Kwa mujibu wa Dkt Mwasaga ziara hiyo ni moja ya matunda ya makubaliano yaliyosainiwa mwaka jana baina ya serikali za Tanzania na Estonia kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika eneo la TEHAMA.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara, Dkt Godwill Wanga ambaye ni miongoni wa wajumbe katika ziara hiyo, amesema ziara hiyo ya kujifunza imemwongezea maarifa kuhusu masuala yanayohusu TEHAMA.

“TEHAMA ni nyenzo muhimu sana katika kuchagiza maendeleo na ustawi wa jamii na uchumi kwa ujumla wake. Kupitia ziara hii ya siku tano ya kujifunza naamini nitakuwa nimejengewa uwezo mkubwa,” alisema Dkt Wanga.

"Wenzetu Estonia wamepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwenye tasnia ya TEHAMA. Tuna mengi ya kujifunza nah ii ziara ya kujifunza itatuongezea ufanisi mkubwa kwa watendaji na kukabiliana na uhalifu wa kimtandao," Dkt Wanga.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita kipaumbele chake kikubwa ni kuona TEHAMA inachangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kwani ndiyo mtazamo na mwelekeo wa dunia.

Tume ya TEHAMA ni Taasisi ya Serikali iliyokasimiwa jukumu la kuhamasisha maendendelo ya TEHAMA sambamba na kukuza uwekezaji na maendeleo ya tasnia hiyo hapa nchini.

Wajumbe kutoka Tanzania ambao wapo kwenye ziara ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na usalama wakifuatilia mada ikitoleo na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Estonia Jijini Tallinn jana. Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt Nkundwe Moses Mwasaga.

Wajumbe kutoka Tanzania ambao wapo kwenye ziara ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu wa kimtandao na usalama wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi Dkt Nelle Leosk(wa sita kushoto) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Estonia Jijini Tallinn jana. Wa sita kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt Nkundwe Moses Mwasaga.

Source: https://issamichuzi.blogspot.com/